Tuesday, November 26, 2013

Rais wa TBF Mussa Mziya akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mustakabali wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania.

Shirikisho la Mpira wa kikapu Tanzania leo limetangaza kuhairisha Mashindano ya Taifa Cup ambayo yalipangwa kufanyika Mkoani Mbeya kuanzia Decemba 30'2013 kutokana na Ukata wa fedha kwa ajili ya kuendesha Mashindano hayo.

Pamoja na Mashindano hayo ambayo yalipangwa kwenda sambamba na Vikao vya Bodi ya Shirikisho,Mkutano Mkuu na Uchaguzi wa  Shirikisho la Mpira wa Kikapu navyo vitakuwa vimeathirika na hivyo itapangwa tarehe nyingine na mahali pengine patakapo fanyika Vikao hivyo.

Soma Taarifa Kamili iliyotolewa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania Mussa Mziya
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania akiongea na waandishi wa Habari leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Michezo la Taifa,akiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TBF ndugu Michael Maluwe.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wanahabari,

Kwa muda sasa kumekuwa na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kuhusiana na maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu nchini na mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa Shirikisho. Leo tumeona ni vizuri tutolee ufafanuzi rasmi taarifa hizi.

Kwa niaba ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) napenda nichukue fursa hii leo kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya shughuli mbalimbali za Shirikisho na mchezo kwa ujumla kama ifuatavyo:

1.   Safari ya timu teule ya vijana kwenda Marekani
Wote tunafahamu kuwa Serikali ilikubali na kugharamia kumpata kocha wa kigeni wa mpira wa kikapu kuanzia Janauari mwaka huu. Kocha huyo Albert Sokaitis kutoka Marekani aliingia mkataba na TBF kwa niaba ya Serikali na kuanza rasmi kazi yake ya kufundisha na kuweka program mbalimbali za kuendeleza mchezo wa kikapu nchini.

Moja kati ya mambo aliyoyafanya Kocha katika program yake ilikuwa ni kuteua timu ya vijana, kuwanoa kwa muda na kisha vijana hao waende Marekani ambako wangepata mafunzo ya hali ya juu ya wiki 2. Gharama za safari hii ilikuwa zigharimiwe na TBF kwa upande wa nauli ya kwenda na kurudi na wadau wengine huko Marekani kwa upande wa vifaa, malazi, chakula na usafiri wa ndani, ambao kwa upande wao walisha andaa yote hayo.

Kwa bahati mbaya, wakati Kocha anapendekeza safari hii kwa vijana, bajeti kwa ajili ya kazi zake hapa kwa mujibu wa mkataba ilikwishatolewa na Serikali na hatukuwa na fungu lolote kwa ajili ya nauli kwa vijana hawa. Juhudi za TBF kupata fedha kwa ajili ya nauli kwa timu haikuzaa matunda mpaka tarehe ya safari. Hivyo tuliwasiliana na Kocha kuomba kuahirisha safari mpaka wakati tutakapopata fedha. Kocha ametupangia nafasi mwezi March 2014 kwa safari hiyo

TBF kwa sasa tunafanya juhudi kwa kushirikiana na mamlaka husika kuweza kupata fedha hizo na timu iweze kusafiri hapo mwezi March kama ilivyopangwa.

2.   Azma ya Kocha kujiuzulu

Kumekuwapo na taarifa pia kuwa Kocha Albert Sokaitis kujiuzulu kufanya kazi ya kufundisha na kuendeleza mpira wa kikapu Tanzania. Ni kweli Kocha alitoa tamko hilo la kujiuzulu, lakini hii ilitokana na kuvunjika moyo kwake kwa kushindwa kwetu kuwezesha vijana hawa kusafiri kama alivyopendekeza. Lakini kama nilivyosema awali kuwa jambo hili lilikuwa juu ya uwezo wetu kwa wakati ule kutokana na kuwa zilihitajika takriban Sh. Milioni 50 kwa ajili ya nauli zao, fedha ambazo TBF haikuwa nazo.

Hata hivyo, kwa kuwa suala hili la kuwepo kwa Kocha hapa ni la kimkataba zaidi, TBF kwa kushirikiana na mamlaka husika tulilifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo (kwa simu) na Kocha ili kupata ufumbuzi.

Baada ya mkutano huo na mawasiliano yaliyofuatia kikao hicho, tumekubaliana na Kocha kuwa ataendelea na kazi hii kama tulivyokubaliana awali. Tayari Kocha ameshawasilisha mapendekezo yake na program ya mwaka kwa uratibu na utekelezaji. Vilevile Kocha anaendelea kutuma vifaa mbalimbali ikiwemo mipira kwa ajili ya vijana wetu.

3.  Mashindano ya Taifa Cup 2013

Shirikisho lilipanga kufanya mashindano ya Taifa Cup mwaka huu jijini Mbeya baada ya mkoa wa Mbeya kuomba kuyaandaa nasi kukubali ombi lao. Yalipangwa kufanyika kuanzia tarehe 28/11/2013 mpaka 8/12/2013 na kufuatiwa na mikutano ya Shirikisho na Uchaguzi mkuu wa TBF.

Kwa bahati mbaya, kutokana na sababu zifuatazo, na baada ya mashauriano na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TBF, natangaza kwamba mashindano haya sasa yameahirishwa mpaka hapo itakapotangazwa tena.

(i)           Ukosefu wa fedha za kutosheleza kuendeshea mashindano sambamba na mikutano na uchaguzi wa Shirikisho. Kwa uchache tulihitaji si chini ya Sh. Milioni 10.
(ii)          Wenyeji mkoa wa Mbeya kuomba kuyaahirisha kutokana na kutokamilika kwa wakati kwa viwanja vitakavyotumika kwa mashindano hayo.
(iii)        Mikoa michache kuthibitisha kwa maandishi ushiriki wao katika mashindano.

4.  Mkutano Mkuu na Uchaguzi Mkuu wa TBF

Ndugu Wanahabari, mwaka huu ni mwaka wa mwisho wa kipindi cha uongozi kwa viongozi wa TBF walio madarakani kwa sasa. Hivyo kuwajibika kuwa na uchaguzi mkuu wa viongozi wa Shirikisho, sambamba na mikutano ya Bodi ya Shirikisho na Mkutano Mkuu wa wanachama wetu (vyama vya mikoa vilivyosajiliwa).

Mikutano yote hii na uchaguzi vilipangwa kufanyika sambamba na mashindano ya Taifa Cup yaliyokuwa yafanyike Mbeya kuanzia tarehe 28 Novemba mpaka 8 Desemba 2013. Kwa bahati mbaya tena, kutokana na kuahirishwa kwa mashindano ya Taifa cup, kumeathiri pia na kulazimika kuahirisha shughuli hizi za mikutano na uchaguzi huko Mbeya. Shughuli hizo sasa zitafanyika katika tarehe na mahali patapopangwa baadae na Kamati ya Utendaji ya TBF lakini ndani ya mwaka huu wa 2013. Shughuli za utoaji wa fomu kwa wagombea bado inaendelea na inaratibiwa na Baraza la MIchezo la Taifa (BMT). Hivyo wote wanaotarajia kugombea katika nafasi zilizotangazwa awali katika uchaguzi huo wanaombwa waendelee kuchukua fomu.

Imetolewa na
Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF)